Sasa ni rasmi, waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa ndiye mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Chadema. Mwanasiasa huyo mkongwe na ambaye amekuwa gumzo ndani ya CCM,
alikitosa chama hicho na kujiunga na upinzani.
Baada ya kujiunga na Chadema, alichukua fomu za
kugombea urais na kudhaminiwa na wanachama wapatao 1.6 milioni. Jana
alitambulishwa na kupitishwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Chadema pamoja na
mgombea wake mwenza, Juma Duni Haji.
Wagombea wote wawili ni wapya.
Wakati Lowassa akipokewa kutoka CCM, Juma Duni
amejiunga Chadema akitokea CUF katika mkakati maalumu kwa makubaliano ya
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akiwa CCM, Lowassa alikuwa kada wa kwanza
kutangaza nia ya kuwania urais Mei 30 katika mkutano wa hadhara
uliohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid,
Arusha.
Katika mkutano huo Lowassa alikumbushia tukio la
mwaka 1995 alipojitokeza kugombea urais pamoja na Rais Jakaya Kikwete
akisema, “Natarajia safari hii (mwaka 2015), Kikwete ataniunga mkono.”
“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana.
Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na
waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo
halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita
kati yetu, mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.”
Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye alichaguliwa
kuwa mbunge mwaka 1990, ni kati ya watiania wa CCM walioibua mvutano
mkali katika mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake, huku akiungwa
mkono na idadi kubwa ya wabunge, viongozi wastaafu wa chama hicho na
wenyeviti wa wilaya na mikoa wa CCM. Hiyo ndiyo sababu ya kutoa kauli za
kujiamini.
Asiyenipenda CCM aondoke
Akizungumza mjini Dodoma Mei 25, Lowassa alisema
iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa
sababu yeye hana mpango huo. “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina
Plan B, mimi ni Plan A tu, tangu nimemaliza chuo kikuu mwaka 1977,
nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo
nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha
(AICC). Maisha yangu yote yapo CCM. Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani
ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Sina mpango wa kushindwa
Mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa
kuwania urais kupitia CCM mjini Dodoma Juni 5 mwaka huu, Lowassa alisema
hana mpango wa kushindwa. “Swali rahisi sana, sina mpango wa
kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na
waandishi wa habari kama ana mpango mbadala ikiwa angeenguliwa na CCM.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya uchukuaji wa fomu, Lowassa aliyekuwa
akijibu kwa kifupi maswali ya wanahabari, alisema kama kuna mtu ana
ushahidi na tuhuma za ufisadi dhidi yake ajitokeze hadharani. “Kama
hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme, na anitaje.
Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi,”
alisema.
Alipoulizwa kuhusu uteuzi wa baraza lake la mawaziri iwapo atakuwa rais, Lowassa alisema, “Nitavuka daraja nitakapolifikia.”
Kwa mapokezi haya nimeshashinda
Juni 6 mwaka huu akiwa mjini Mwanza kusaka
wadhamini, Lowassa alianza hatua hiyo ya mwisho ndani ya CCM kuelekea
kugombea urais kwa kupata mapokezi makubwa yaliyomshawishi kusema; “Kama
ni mpira, tayari nimeshinda kwani sijawahi kupata mapokezi makubwa kama
haya Mwanza. Nina sababu kuu mbili za kusema kwamba nadeka na kama ni
mpira nimeshinda. Mapokezi niliyoyapata hapa Mwanza hayajawahi kutokea,
lakini hii ni faraja kubwa ya pekee kwangu,” alisema Lowassa baada ya
kukabidhiwa fomu hiyo.
“Leo sitasema sana, lakini nawaomba wanaccm
tujenge mshikamano wa pamoja kukabilina na vita ya watu watakaokomba
rasilimali za Taifa.”
Pia, alisema Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakuwa
mgumu tofauti na uliopita na kwamba, ni mtihani kwa CCM kuteua mtu
makini atakayaweza kulinda rasilimali za nchi. Lowassa alisema huu ni
wakati wa CCM kujenga mshikamano wa pamoja na kukabiliana na watu ambao
wanaweza kukomba rasilimali za nchi.
Muda wa mabadiliko umefika
Juni 20, Alikuwa mjini Iringa ambako alisema kuwa
muda wa mabadiliko aliyotabiri Mwalimu Julius Nyerere ni sasa na kwamba
yeye ndiye anayeweza kuyaongoza. Alisema kwa sasa CCM inahitaji
mabadiliko makubwa na akanukuu kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka
1995 alipozungumzia haja ya chama hicho kujisahihisha.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji
mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,”
alisema mbunge huyo wa Monduli kwenye mkutano huo uliofanyika Uwanja wa
Samora mjini Iringa. “Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga
inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,”
alisema.
Lowassa alisema aliamua kuingia kwenye mbio za
urais kwa sababu tatu: Kufanya mabadiliko ndani ya CCM, kufanyia kazi
tatizo la umaskini na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana.
Hakuna wa kumkata
Juni 22, akizungumza mara baada ya kuwasili
mkoani Ruvuma alisema hatarajii jina lake kukatwa katika vikao vya CCM
vitakavyoketi kumteua mwanasiasa atakayepeperusha bendeara ya chama
hicho katika kinyang’anyiro cha urais.
“Nimekuwa mwanaccm tangu mwaka 1977 nilipomaliza
chuo kikuu, sijawahi kufanya kazi nje ya CCM, hivyo nakijua chama na
hakuna mgombea atakayeweza kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika
chama, sasa leo anayetaka kukata jina langu anatoka wapi? Anakata kwa
sababu gani? Sioni kosa la kukatwa jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo
msiwe na wasiwasi jina litarudi tu,” alisema.
CCM ikijipanga itashinda
Juni 25, alikuwa mjini Babati na kusema iwapo
CCM itajipanga vizuri ikamaliza migogoro na kujiamini, itashinda mapema
katika uchaguzi. “Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha ugomvi katika
umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu,”
alieleza. Alisema iwapo jina lake lingepitishwa, uchaguzi mkuu ungekuwa
umekwisha mapema kutokana na kuwa na ushawishi mkubwa kwa wapigakura
nchini.
Pamoja na kauli hizo jina la Lowassa lilikatwa
tena katika hatua ya awali kabisa. Kamati ya Maadili na Usalama ndiyo
ilifyeka jina lake wakati kanuni zinataka kamati hiyo iwasilishe majina
kwa Kamati Kuu yenye jukumu la kukata. Mzozo umeanzia hapo. Hasira
zilionekana hapo na mpango mbadala ambao hakuwa nao ulianza kujengwa
hapo.
Mpango B
Kutokana na kujiamini sana, Lowassa hakuwa na
mpango mbadala hivyo alitoa kauli hizo akidhani makubaliano yake na Rais
Kikwete ya mwaka 1995 yangeheshimiwa. Alipata nguvu wabunge
waliposhangilia kwa nguvu Rais Kikwete alipomshukuru kwa utumishi wa
miaka miwili kama waziri mkuu. Hata hivyo, alipokatwa alilazimika
kuungana na waliokuwa maadui wake kisiasa, Chadema ili kufufua safari
anayoiita “ya matumaini”.
Utumishi wake
Katika miaka miwili ambayo amekuwa waziri mkuu,
Lowassa alionyesha mfano wa namna ambavyo mtendaji na msimamizi mkuu wa
shughuli za Serikali anavyopaswa kuwa. Lowassa alikuwa mfuatiliaji.
Aliwafuatilia kwa karibu wakuu wa mikoa na wilaya na wakurugenzi hadi
akafanikisha ujenzi wa shule za sekondari za kata, na uboreshaji wa
barabara za jiji la Dar es Salaam.
Pia, amekuwa kiboko cha wawekezaji wababaishaji.
Mwaka 2003 alipokuwa Waziri wa Maji aliifutia mkataba kampuni ya City
Water Services.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano; wasichana wawili na
wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na
Richard.
Post a Comment